​TUNAWASUBIRI ITALIA WARUDI ILA WAO WANAITAMANI HADHI YA EPL

MIAKA kadhaa iliyopita tulikuwa tunasema Serie A ni ligi ya viatu, undava sana. Sasa hivi tunaburudika na mabao matamu tu.
Miaka kadhaa nyuma ilikuwa ukiulizwa uchague kati ya kuangalia muvi ya Denzel Washington au kucheki mechi ya Lazio na Napoli, utachagua muvi.

Siku hizi, kila Jumamosi hata kama unaambiwa kuna harusi yenye bia za kumwaga na jioni kuna mechi ya Atalanta na AC Milan, utabaki kuangalia mechi.

Siku hizi vita imekuwa ya wote pale Italia.

Kipindi fulani ilionekana kama ni ‘tusi’ kusema Serie A ni ligi ya tatu kwa ubora wa soka barani Ulaya. Ila ukweli ulijulikana wazi. Kwanza imetoa timu zilizocheza fainali za michuano ya Ulaya mara 12 kati ya 1983 na 1998.

Italia walipigwa kumbo kwenye eneo moja tu. Masuala ya kifedha. Kiuchumi hawakuwa sawa. Hapa kweli waliangushwa na mikataba ya TV isiyokidhi hadhi yao.

Serie A iliachwa mbali sana na Premier League. Hadi sasa bado wanajikongoja.

Timu za England zinalipa mishahara mikubwa ambayo hakuna mmiliki wa klabu yoyote ya Italia mwenye uwezo wa kujitutumua na kutoa. Wakijitutumua sana kwenye usajili ndiyo wataweza kutamba.

Upande mwingine, Barcelona na Real Madrid nazo zikatumia vizuri sana michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kujijengea majina yao duniani. Halafu zile timu za Serie A zilizokuwa zikijiweza kiuchumi, zikihangaika na ile skendo ya upangaji matokeo ya Calciopoli na kujikuta hata Bundesliga nao wakikwea juu yao katika ubora wa soka Ulaya.

Angalau, miaka takribani mitano hivi hapo nyuma ndiyo nguvu ikaanza kuongezeka. Tukaiona Juventus ikitesa kwa misimu sita mfululizo.

Ila sasa hivi si unaona jinsi wanavyoisoma namba. Sasa hivi kiti chao cha ufalme huenda kikachukuliwa na mojawapo kati ya Napoli au Inter Milan. Hizo ndizo timu ambazo hazijapoteza mchezo wa Serie hadi kufikia jana.

Zamani wachezaji vijana kutoka kila kona ya dunia walikuwa hawana hamu ya kwenda Serie A. Siku hizi wanapata na hamu ya kuvunja rekodi za wahenga waliowahi kuacha alama Italia.

Wachezaji waliokuwa wanaonekana mizigo kwenye timu kubwa, ndio hawa wanaokimbiza kila michuano wakiwa na timu za kawaida tu.

Juventus ilifungwa wikiendi iliyopita na Sampdoria, watu wakachukulia poa kwa kuwa ni ligi isiyofuatiliwa na wengi. Lakini pale Sampdoria kuna kijana Lucas Torreira ambaye anamulikwa kama dhahabu inayosubiriwa kuling’arisha taifa la Italia.

Nenda Fiorentina, utakutana na Federico Chiesa mwenye umri wa miaka 19 tu. Rudi Milan, ambao wametumia zaidi ya euro milioni 200 kwenye usajili mwaka huu ila wachezaji waliocheza vizuri zaidi ni makinda waliotoka akademi, Gianluigi Donnarumma, straika Patrick Cutrone.

Majirani zao, Inter ndio wanaotisha msimu huu. Tenga muda wako uione Inter ya Luciano Spalletti inavyopiga mpira mwingi na akina Mauro Icardi, Ivan Perisic anayeliliwa na Man United hadi leo. Halafu cheki safu yao ya ulinzi, yenye watu kama Roberto Gagliardini na Milan Skriniar.

Serie A siku hizi ina timu zinazofunga sana mabao. Zina washambuliaji hatari sana hata Ulaya. Mcheki Dries Mertens, ni kifaa kinachotikisa. Tangu kuanza kwa mwaka huu, Mertens ametupia mabao zaidi ya 20 na pasi za mabao zaidi ya 10.

Nenda Lazio kuna Ciro Immobile. Torino wana Andrea Belotti.

Nadhani hadi sasa umeshapata mwanga wa namna soka la hadhi ya juu Italia linapoelekea. Linapita kwenye njia sahihi. Kwa manufaa ya ligi. Ila itakuwa na faida gani kwa timu yao ya taifa?

Wachezaji wote hao uliotajiwa si kwamba wanawafurahisha mashabiki tu. Kuna mabosi wa Serie A wenyewe wanafurahi tu kuona vyombo vya habari vikiwafuata wachezaji wao mara baada ya zile mechi za michuano ya Ulaya.

Wanafurahi kwa sababu ligi yao itatangazwa sana. Na lazima wachezaji wazuri watavutiwa kwenda huko. Baada ya hapo mashabiki watavutika viwanjani. Vuta picha viwanja vya San Siro na Olimpico vikijaza maelfu ya mashabiki, vipato vitaongezeka.

Baada ya miaka kadhaa nini kitatokea, ni utitiri zaidi wa wachezaji bora. Kila mtu atageuzia macho Italia. Nadhani umeipata picha kwa uzuri sasa.

Lakini, ukigeuka nyuma ndipo utakapogundua akina Curtone, Alessio Romagnoli, Jorginho, Marco Benassi na Domenico Berardi na wengineo ambao hawajafikisha hata miaka 28 na wanataka kutamba kwenye ligi ya kwao, wakiozea benchi.

Wataisaidiaje timu ya taifa kama hawachezi? Serie A ndio kwao, kwa muda mrefu Italia imekuwa ikitumia wachezaji kutoka kwao, asilimia 90 ya wachezaji wao wa taifa hutokea nyumbani.

Milan inapotaka kumnunua mtu kama Willian, ifikirie kuna kiungo mzuri tu, Manuel Locatelli ambaye anaozea benchi.

Unadhani winga Willian atawezaje kucheza na Locatelli wa miaka 19 ambaye alishaonesha ari na utayari wa kucheza soka la wakubwa. Lazima atataka kucheza na supastaa mwenzake, Hakan Calhanoglu. ambaye naye anangojea nafasi kwa Suso.

Unaweza kuona jinsi gani ambavyo Italia inatamani ifikie hadhi ya EPL kwenye suala la kuwa na ligi maarufu lakini, ni jambo ambalo litaathiri mipango yoyote ambayo watajiwekea kwa ajili ya kuiinua timu yao ya taifa kutoka kwenye anguko la soka kimataifa.

Hakuna jinsi, itabidi tuwasubiri tena baada ya miaka isiyohesabika.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s