MBARAKA, KIINGILIO CHETU NI ‘BUKU’ TU

Na Kelvin Lyamuya

DAKIKA zilikuwa zinaenda kasi sana usiku wa kuamkia jana hadi nikajikuta natamani lile pambano la Wladmir Klitschko na Anthony Joshua lingekuwa refu.

Kwa Klitschko, pambano lile angelingemaliza kwa uzoefu, lakini AJ akasaidiwa na nguvu alizonazo, umri wa kupambana na akili inayowaza kufika mbali kama alipofikia mwalimu wake Klitschko.

AJ ni bondia anayependa kujifunza. Alijifunza vitu mbalimbali kutoka kwa Klitschko na raundi 11 alizotumia kupambana naye juzi zilimfunza mengi pia.

Kwenye soka pia wapo vijana kama AJ. Kwao kupambana na kujifunza mbele ya wachezaji wazoefu ni kanuni isiyotakiwa kupuuzwa.

Yupo Marco Asensio. Yupo Marcus Rashford, pia Kylian Mbappe ambao umri wao haupishani sana na yule Mbaraka Yusuph.

Straika mdogo anayechuana na wazoefu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye orodha ya ufungaji bora.

Nilipomuona uwanjani nikatamani nimuone kwa macho yangu. Je, ubabe wake kwa mabeki hadi kufikisha mabao zaidi ya 10 kwenye ligi unaendana na anachokifikiri kwa ajili ya maisha yake ya soka la baadae?

Je, anaizingatia kanuni ya kujifunza kutoka kwa washambuliaji wakali waliopo kwenye timu mbalimbali?

Nilipobahatika kumuona na kumsikiliza kwa umakini, nikagundua anahitaji msaada mkubwa kufika mbali kisoka.

Iwapo anatakiwa na Simba na Yanga, atambue hizi ni timu zenye hadhi kimataifa, lakini zinatia shaka kimataifa! Awe makini mno.

Mbaraka ni mshambuliaji anayestahili kucheza nje ya Tanzania, ni haki yake kabisa. Lakini kutoka Kagera na kukimbilia kwa haya majabali bila kufikiri mara mbili itakuwa ni hatari kubwa kwake. Nakithamini sana kiwango chake.

Ubora wake wa kufumania nyavu ndio unaosakwa na maskauti pale Afrika Kusini, DRC, Ghana, Ivory Coast na kwingineko. Asijaribu kupoteza muda na bahati kwa kukimbilia Jangwani na Msimbazi.

Kwanini nasema hivyo?

Ninao uhakika, Mbaraka anafuatilia Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Iwe ni mahala kokote tu anapopenda yeye, lakini ufuatiaji wake kwenye soka hauna tofauti na sisi tunaojikongoja taratibu usiku wa Jumanne au Jumatano kwenda kuitazama mechi ya UEFA na ‘buku’ yetu mikononi.  Kiingilio chetu wananchi wa Tanzania tunaotamani maendeleo yetu kisoka yafikie kiwango angalau cha wenzetu.

Ninao uhakika, Mbaraka ameona yanayofanywa na Mbappe pale Monaco ambaye miaka mitano iliyopita aliwahi kupiga picha ya pamoja na Cristiano Ronaldo, mtu anayetajwa kuwa ni mfano wake wa kuigwa.

Kwanza alikuwa ni mdogo sana, lakini alionesha furaha kukutana na staa wa dunia, na sasa anaifanya dunia ya soka ikae na kumzungumzia Mbappe wa miaka 18.

Tayari ameshaweka rekodi mbalimbali na umri wake mdogo tu kwenye soka. Kijana mdogo zaidi kufunga kwenye robo fainali na kufikisha mabao 15 ya Ligue 1 kule Ufaransa katika karne hii ya 21!

Ni faida kubwa kwa Mbappe. Baada ya kujitambua alihitaji nini katika maisha yake ya soka, sasa anafaidi matokeo ya uamuzi wake wa kubaki Monaco kipindi saini yake ilipokuwa ikigombaniwa.

Mbaraka, umri wako ni tunu yetu kwa sasa na tuna imani utaleta faida hapo baadae katika mashindano mbalimbali na Taifa Stars, hata kwa Kagera Sugar.

Na sio wewe peke yako, wapo wengine. Yusuph Mhilu, Ayoub Semtawa, na hata Shiza Kichuya.

Muda ulionao ni mzuri wa kutimiza yale uliyoyakusudia. Kikubwa ni kujiheshimu na kutambua unachopaswa kukifanya uwanjani na nje ya uwanja.

Wakati utafika na utaweza kuamua wapi uende ili utimize malengo yako, unahitaji washauri wazuri kufanya hivyo.

Kuna kipindi mwaka huu Mbappe hakutaka kuhamia Real Madrid, si kwamba anaogopa ila anatambua muda wake wa kucheza na kujinoa zaidi upo Monaco, Madrid ni kubwa kwake. Amejifunza kwa Anthony Martial.

Akili yako Mbaraka iwe ndio ofisi yako, itumie vizuri kujitathimini kabla ya kufanya maamuzi ya kutoka Kagera Sugar, huenda ukaiacha bahati nzuri hapo kama hii aliyonayo Mbappe ambaye anafaidi matunzo anayopata pale Monaco.

Na ukumbuke una deni langu, uliniahidi kuongeza idadi ya mabao kabla ya msimu kumalizika. Naamini unao uwezo wa kufanya hivyo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s