TUMUACHE GUARDIOLA ACHANGAMSHWE UBONGO

Na Kelvin Lyamuya

WAKATI nikiendelea kumfuatilia Pep Guardiola, nimegundua sasa kichwa chake kilichojaa falsafa na ufundi wa kimbinu alioambukizwa na Hayati Johan Cruyff, kimeanza kuchangamka.

Pamoja na ‘U-master’ wake tangu akiwa Barcelona hadi Bayern Munich, na kujipatia umaarufu mkubwa. Kuogopeka na makocha wenye hadhi, bado akili yake ilihitaji kunolewa zaidi.

Ubongo wake uliobarikiwa kuelewa nini kinachohitajika kwenye mchezo mzima ulitakiwa kupata changamoto mpya. Dhidi ya timu mpya, zinazotumia mbinu ngumu. Alihitajika England, na swali moja tu ambalo mwenye hofu angejiuliza ni kwamba ligi yenyewe itampokeaje?

Wakati ambao tulizoea kusikia makocha wa EPL wakilalamikia ugumu wa ratiba hasa inapofikia kipindi cha sikukuu, ndio muda ambao Guardiola alikuwa akiutumia kujipumzisha kwenye jua safi lenye afya la Doha, Qatar, Uarabuni huko. Wenzake walipokuwa wakitaabika, yeye aliupata upepo mwanana huku akitafakari namna ya kuisuka Bayern imara zaidi kwa ajili ya nusu ya pili ya msimu. Bayern ikabeba tena kombe la Bundesliga wakati baadhi ya wenzake wakiumia na ugumu wa ligi!

Hapo ndipo kipande kidogo cha dunia ya soka kiliposikia Guardiola akisifiwa mno, akiheshimika mno, kikakataa kukubali. Kikagoma kabisa kufuata mkumbo wa kusifu bila kujiridhisha kwa asilimia zote. Kikamhitaji Pep aje. Aje awaoneshe na huku uwezo wake.

Alipofika sasa kila mtu akawa na shauku ya kuona kitakachotokea kwa sababu ni lazima kungetokea mgongano wa vitu vingi; falsafa za soka na tamaduni ingekuwa tofauti. Kwa kuwa yeye alishazoea kusimamia anapopaamini ndio maana watu walimtaka aje kwenye ligi isiyotabirika, ligi yenye timu zinazoamini mbio na nguvu ndio msingi wa ushindi. Watu walisubiri kuona je, Guardiola aliyezoea soka la pasi fupi fupi na kumiliki mchezo, atachanganywa na presha au itamkomaza?

Akiwa Bayern, aliifanya ile timu kucheza aina nyingine tofauti kabisa na ile ya Jupp Heynkes. Ni katika kipindi ambacho ndio alitoka Barca na kuingia Ujerumani. Watu walimsubiri kwa hamu kuuona ubora wake nje ya Hispania na alichokifanya ni kupachika kanuni yake ya pasi 15. Kwa kiasi kikubwa hii ilikuwa ni kanuni ngeni kwa Bayern, kuanzisha mashambulizi kuanzia kwa beki, kupitia kwa viungo na kwa kasi zaidi kuelekea kwa mafowadi lilikuwa ni jambo ambalo halikuzoeleka. Bayern ilicheza sana soka la kuonekana kwa macho ya kawaida. Watu walipenda hivyo tu.

Lakini mwisho wa siku ni nini? Bayern ikawa timu yenye nguvu zaidi, kiujumla ilipata dawa dhidi ya timu za Ujerumani ambazo zilipendelea ‘counter-pressing game’. Mashambulizi ya haraka kwa kutumia makosa ya mpira uliopotezwa. Nilishuhudia Guardiola akiifanya Bayern iwe na uwezo wa kumaliza mchezo huku safu yake ya ulinzi ikitumia muda mwingi kwenye nusu ya eneo la mpinzani. Hapa na mimi nilianza kumtamani Guardiola, sikuwa na uhakika ni lini aje, ila kwa muda wake angeamua aje lini. Lakini alitakiwa kuja, lazima.

Kuna ukweli ambao ni mgumu kuukataa. Mbinu za Guardiola huwa hazikosi lawama. Kuna wanaosema aina ya soka analofundisha huwa ‘linaboa’. Anaweza akachezesha mtu mwingine wa ziada kwenye eneo ambalo wewe utaona hakuna ulazima, lakini ndivyo anavyoamini, na ndivyo soka la kisasa linavyohitaji, mbinu zako hukupa nafasi ya kuusoma vizuri mchezo kadri unavyoenda na nini kitakachohitajika.

Alichoshindwa tu ni kuitengeneza Barcelona ‘toleo la pili’ pale Munich. Kiufupi, kile kilichohitajika Ujerumani ni tofauti na Hispania, utambue hilo, Bayern walitaka makombe muhimu na sio burudani ya soka la uwanjani. Japokuwa hakuweza kuwapa Uefa (walilitamani sana), akaweza kuingiza falsafa yake.

Akiwa City, anahitaji muda tu hadi atakapofanikiwa kuingiza falsafa yake. Lakini kwa sasa acha ubongo wake uendelee kuchangamshwa kwanza na tungo za soka la nguvu na mbio.

Hispania alichezesha soka la Salsa laini. Ujerumani akukutana na ladha ya soka la ‘Heavy Metal’, lakini sio gumu kama England ambako ni mchanganyiko wa fujo za Rock na Heavy Metal!

Aheshimiwe kwa kubeba makombe matano ya ligi kuu mbili kubwa, ndani ya miaka saba ya kufundisha soka la ngazi ya juu Ulaya. Kama kuiteka Ligi Kuu ya England, tumtunuku muda zaidi kwanza kwani hatukujua ligi yenyewe ingempokea vipi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s