Wenger anajiongezea madeni yasiyo na ulazima Arsenal

Na Kelvin Lyamuya

WATAALAMU wa mambo wanasema kama unataka kushughulikia tatizo ni heri ukawa na uhakika wa tatizo lenyewe kama lipo. Hivyo kwa kile alichodai Arsene Wenger kwamba Arsenal ipo kwenye ‘wakati mzuri’ baada ya kile kichapo cha mabao 10-2 kutoka kwa Bayern huenda akawa ametambua nini shida. Pia mzee huyu ni kama amewazaba kofi mashabiki waliomfukuza kazi kwa mabango hivi karibuni.
Kwa namna moja au nyingine, Wenger yuko sahihi. Kwa sababu ukiitazama Arsenal haina tatizo la kifedha, na takribani miaka 20 wamefanikiwa kumaliza ndani ya nafasi nne za juu kwenye ligi kuu. Lakini kama mwenyekiti wa klabu Stan Kroenke atakuwa anaamini kwamba makombe ni kitu cha nyongeza, basi mashabiki nao wana haki ya kuhuzunika na kutoa dukuduku lao.
Wakitazama kabati lao la makombe lina mataji mawili ya FA ndani ya miaka 11. Wanashangaa ni kocha gani ambaye angekaa kwa muda mrefu na mataji machache hivyo, na huku bado akiendelea kupewa mkataba mpya.
Sasa hivi hamu yao ni kumuona Wenger akiondoka. Lakini kusikia kwamba mzee huyo ataongeza mkataba kutapelekea awe na deni kubwa kwa mashabiki, deni la kubadilika na kuondoa nuksi ya kushindwa kila mwaka, ataweza?
Zamani alikuwa na uwezo wa kubadili mambo ndani ya timu. Alipoingia England kwa mara ya kwanza aliifanya Arsenal kuwa timu imara kuanzia kwenye uchumi, mbinu za kimchezo na hata maisha ya wachezaji kuzingatia afya, mlo. Hiyo ilikuwa zamani sio sasa.
Hapo awali alikuja na ukuta mgumu kwenye ulinzi. Safu iliyokuwa ikiongozwa na Tony Adams. Safu hiyo ya ulinzi ndio iliyoifanya Arsenal kutamba na kucheza soka la burudani ambalo halikuwahi kutokea England. Ilikuwa timu ya ushindi.
Baadae akabadilika, akaja na mbinu ya kucheza soka la pasi fupi fupi na za haraka, akidhani kwamba Arsenal sasa ingejipambanua zaidi nje ya England, lakini kumbe Barcelona ndio klabu pekee ambayo ilikuwa na msingi imara wa kucheza soka la aina hiyo. Na ndio timu iliyotawala ulimwengu wa mpira wa miguu kwa burudani ya soka lao.
Na sasa Wenger anatakiwa kubadilika tena. Ila changamoto kubwa kwake ni kwamba upinzabi umekuwa mkubwa. Zile timu ambazo kipindi kile alikuwa na uwezo wa kukabiliana nazo, zimeimarika sana.
Zimekuwa na nguvu ya usajili, makocha wapya wenye mawazo mapya. Wenye kuleta changamoto mpya.
Kocha kama Antonio Conte amekuja na mfumo wake 3-4-3 ambao umeibadili Chelsea kutoka Twiga wapole hadi Simba asiye mkubwa wa mwili lakini anatingisha msitu. Nani aliyewahi kudhani Victor Moses atakuja kuwa mtu muhimu pale Chelsea? Makocha wengine, Pep Guardiola, Mauricio Pochettino, Jurgen Klopp na Jose Mourinho pia wamekuja na mbinu mpya, lakini ni Wenger ambaye bado anaamini kile alichokuwa nacho kwa miaka yote hiyo.
Hata wachezaji wake ni wale wale, lakini hali inapoelekea huko itazidi kuwa ngumu kwake. Mashabiki wameshapoteza imani naye. Wachezaji wake nyota Alexis Sanchez na Mesut Ozil mikataba yao inakaribia kuisha na ana jukumu la kutafuta warithi wa wachezaji muhimu mno, Santi Cazorla, Laurent Koscielny na Petr Cech ambao umri wao unaelekea kuwatupa mkono.
Wenger hatakuwa mpumbavu kwa kujilazimisha kuishi kizamani kwenye dunia ya kisasa. Anajua changamoto iliyopo, lakini dalili za kweli kama atafanya mabadiliko huenda zikachukua muda mrefu zaidi ya miaka atakayotumia kiungo Granit Xhaka kuzoea mfumo wao.
Kwa sasa ana miaka 67, na ukweli ni kwamba yeye sie kocha sahihi wa kubadili hali ya Arsenal. Ni Arsenal kufanya mabadiliko ya kocha, ndipo Arsenal itabadilika. Kwa sababu kazi atakayotakiwa kuifanya iwapo ataongeza mkataba itakuwa nzito kuliko nguvu aliyonayo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s