GUARDIOLA, ULIKABIDHI FAILI LIPI KWA ENRIQUE?

BARCELONA. Imebadilika. Tena imebadilika sana. Ukizitazama zile bao 4-0 walizopigwa na PSG utagundua mengi kwa jinsi utakavyoichambua.

Barca ya Wakatalunya imebadilika mno. Na mabadiliko yenyewe mengi si chanya.

Najua utajiuliza kwanini si chanya? Kwanza wana kikosi finyu. Hakuna wachezaji wa kutosha wa kupokezana nafasi. Wanaoanza na wanaosubiri wanatofautiana mno kiuwezo.

Kingine wanaitegemea sana MSN. Ule muunganiko wa Messi, Suarez na Neymar. Mpira usipofika kule mbele utawahurumia Barca. Watahaha mno kucheza soka walilolizoea.

MSN ndio washambuliaji na wakati huo huo wanatakiwa kucheza kama viungo. Yaani Messi, Neymar na Suarez wote wanahitajika chini kukaba, kupokonya mipira, wakati huo huo wapandishe mashambulizi juu. Hata kama tunauita utatu mtakatifu wao kuwa ni bora zaidi duniani, hawawezi kufanya yote haya peke yao.

Nikukumbushe fainali yao ya Ulaya dhidi ya Man United iliyopigwa Roma, 2009. Barca ile ilihangaika kuipata ladha yao ya soka ndani ya dakika nane za mchezo. Kila mtu alikuwa kwenye eneo lake lakini hawakuwa na sumu, bado walilala. Waliwaheshimu sana Man United, hawakutaka kuwasumbua.

Ronaldo akawashtukiza na shuti, Victor Valdes akaupangua. Fataki jingine linaachiwa, United wakatawala sana mchezo. Dakika chache, Cristiano kwa mara nyingine akalifumua shuti. Sentimita chache mno zilihesabika kati ya mwelekeo wa shuti lile lililotoka nje na upande ambao Ronaldo alinuia kufunga.

Umeiona tofauti hapo? Ni sentimita chache pembeni kabisa mwa lango. Zilikaribia kubadilisha kauli za dunia ya ulimwengu juu ya Barca iliyokuwa kwenye zama za furaha. Chini ya Pep Guardiola.

Zilikuwa ni dakika tamu za awali, Giggs, Carrick, Anderson wote walitandaza soka la kueleweka muda huo. Najua ulitamani kifanyike kitu pale. Lakini kadiri presha inavyozidi, ndipo Guardiola aliposhtuka. Akainuka na kuanza kuwawapigia sana kelele vijana wake. Alitoa maelekezo kwa kutumia mikono yake kama vile anawatafsiria lugha viziwi!

Sauti yake kali ilipenya kwenye masikio ya wachezaji wake kuliko hata kelele za umati wa mashabiki waliofurika Stadio Olimpico pale Rome. Messi anaambiwa, “Kamata mpira, pangua ngome ya United hiyo.” Alikuwa kama namba tisa, lakini ni namba tisa feki dimbani na wakati huo huo Eto’o anaamrishwa kutokea kulia pembeni kwa kasi na nguvu yake.

Babu yetu mpendwa, Ferguson, alitulia tu kwenye benchi lake. Hana wasiwasi. Bazooka ikiteseka katikati ya meno yake.

Tayari aliridhika na hali ya hewa. Aliona kama kaiweka Barca kiganjani. Kumbe ile si Barca ya mwaka huu, ile ilikuwa ya Pep!

Hali ya hewa ikavurugika. Hakuna aliyetarajia, ni ghafla mno. Pasi zinaanza kupigwa kwa kasi. Messi, Iniesta, Xavi, Messi. Hapo anasikika mtangazaji tu akiwatangaza vijana wa Barca wakipokezana pasi.

Ni hali ya ghafla inayowalazimu Carrick na Anderson kufikiri zaidi nini cha kufanya, kuamua nani wa kumkaba pasi gani iharibiwe, eneo gani linalovunja wa lizibwe haraka. Muda huo, Giggs ameshakamatwa na Busquets na hakuna mwingine wa kuwasaidia zaidi yao.

Rasmi, kiungo cha United kikaingia mikononi mwa maharamia wa Katalunya. Kilichofuatia ni historia ambayo hadi leo tunaikumbuka. Lakini hatuoni kama Barca ile itarudi tena. Mbona jahazi linataka kuzama.

Liko wapi faili aliloliacha Guardiola? Luis Henrique alipewa faili lipi? Mbona anaipoteza Barca? Tuna mashaka kama wataweza kurudisha bao nne.

Alipoondoka Pep, ni wachache waliotumai kwamba Barca ingesalia vile vile. Mimi nilikuwa mmoja wapo kati ya wachache. Ilikuwa ngumu kuamini asilimia mia. Kinachotokea siku hizi ni zaidi ya kile tulichokitarajia.

Barcelona kwa kiasi kikubwa imepungukiwa madini kutoka kwenye kichwa cha Guardiola, sana. Hasa pale inapofungwa.

Uwepo wake ulikuwa muhimu pale, namna alivyokuwa akifiriki ndani ya mchezo na kuifanya timu yake icheze soka la kuvutia bila kupunguza utamu ilikuwa ni kama sukari kwenye kashata.

Alikuwa ni kiumbe maalumu aliyetumia vizuri ushauri wa Hayati Johan Cruyff. Kusaka njia za ushindi nna alipozipata alifanya anavyotaka. Kwa haya yanayotokea, si rahisi kuvumilia. We miss you Pep!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s